Rais Samia: Tumeruhusu mikutano vyama vikue, si kutukana na kuvunja sheria

0
42

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa vyama vya siasa kuzingatia demokrasia ikiwa ni pamoja na misingi ya nchi iliyowekwa na kutumia hoja na fikra zenye tija zinazolenga kuimarisha utendaji serikalini.

Akizungumza katika mkutano maalum wa Baraza la Vyama vya Siasa na Wadau wa Demokrasia uliofanyika jijini Dar es Salaam, amesema dhumuni la kuruhusu mikutano ya hadhara ni kutoa fursa kwa vyama vya siasa kujiinua na kusikilizwa na wananchi wake na si kutumia nafasi hiyo kubomoa misingi ya nchi.

“Yeyote anayeitakia mema nchi hii, atakwenda kwenye misingi hiyo, hatokopi misingi ya anakotoka huko ailete hapa atake tuitekeleza hapana, tuna mila, desturi yetu ya Kitanzania, tutakwenda kwa misingi hiyo,” amesema.

Ameongeza “Tumeruhusu mikutano ya hadhara tukiwa na nia vyama vya siasa vizungumze, wananchi wawasikie sera zao, mada zao, mipango yao ili vyama vikue na virudishe wale waliowapoteza viweze kukurudishwa, vyama visimame viwe madhubuti, tukienda kwenye uchaguzi kila chama kimejijenga vya kutosha.

Rais Samia: Kama mtu amevunja sheria ashughulikiwe haraka

Aidha, Rais Samia pia amesema uhuru wa kutoa maoni kusisababishe udhalilishaji kwa watu wengine, kuibua hisia za kidini, ukabila au kubaguana kwa misingi yoyote ile badala yake utumike vizuri bila kuingilia haki na uhuru wa watu wengine pamoja na kufuata sheria, kanuni na taratibu.

Mbali na hayo, amesema marekebisho ya katiba yameanza kufanyiwa kazi kwa kuzingatia misingi bora ili iweze kuleta manufaa kwa wananchi wote.

“Katiba si mali ya vyama vya siasa. Katiba ni mali ya Watanzania, awe na chama au hana. Hivyo, matengenezo yake yanahitaji tafakuri sana,” ameeleza.

Send this to a friend