Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imeendelea kutatua changamoto za kodi nchini ambapo imeimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato na kuijengea uwezo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na kuimarisha mazingira ya kufanyia biashara nchini ikiwemo kwa kufuta baadhi ya tozo na kuimarisha utendaji kwenye idara ya serikali, wakala na taasisi mbalimbali za serikali.
Ameyasema hayo wakati akizindua Tume ya Rais ya Marekebisho ya Kodi Ikulu, jijini Dar es Salaam ambapo amesema serikali itaendelea kutatua changamoto za kodi ikiwemo kuandaa mifumo inayotenda haki kwa walipaji.
“Tunataka kujenga mfumo wa kodi unaotenda haki, ambapo kila anayestahili kulipa kodi alipe kodi stahiki, na kodi zote zitozwe kwa mujibu wa sheria. Pia tunataka mfumo wa kodi unaochochea ukuaji wa uchumi wa viwanda na utakaochangia ujenzi wa uchumi jumuishi na unaoiwezesha serikali kutimiza malengo yake ya kuleta ustawi kwa wananchi,” amesema Rais Samia.
Ameongeza, “Kodi ilipwe kwa urahisi, kwa kiwango cha juu, yaani mfanyashara mwenyewe alipe kwa kiwango cha juu bila kusukumana ili nchi ikusanye na iweze kuendelea.”
Aidha, Rais Samia amesisitiza kuwa uchumi wa Tanzania unakua sana, lakini haulingani na kinachokusanywa, kwani wanaolipa kodi ni takriban watu milioni mbili, na kuongeza kwamba kodi ndio damu ya serikali, bila kodi serikali haiwezi kufanya maendeleo.