Katika juhudi za kupunguza ukosefu wa ajira nchini Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ina lengo la kuratibu na kuunganisha shughuli zinazofanywa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuingia kwenye mpango wa ajira kwa vijana katika kilimo, Buliding a Better Tomorrow (BBT) ili kuwajengea mwelekeo mzuri vijana nchini.
Hayo yamebaishwa leo katika maadhimisho ya Miaka 60 ya JKT yaliyofanyika katika viwanja vya Jamhuri mkoani Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi.
“Tunaposema tunakwenda kukarabati makambi zaidi, makambi yanayokwenda kurekebishwa mbali na mafunzo ya ukakamavu na kijeshi yataungana na mpango wa BBT ili kuwajengea kesho nzuri vijana na wanapotoka pale wajue wanakwenda wapi na wanakwenda kufanya nini.
Kinyume na sasa vijana wakitoka, kupata nafasi ya ajira wanazubaa mitaani kwahiyo Tunakwenda kuunganisha mpango wa BBT na kinachofanyika JKT ili vijana wawe na mwelekeo mzuri,” amesema.
Picha za matukio ya maadhimisho ya Miaka 60 ya JKT
Aidha, Rais Samia ameipongeza JKT na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kazi kubwa wanayoifanya pamoja na kujitolea kwa taifa katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo na kuahidi kuwa Serikali itaendelea kuwawezesha zaidi ili ziweze kufikia vijana wengi nchini na kutoa mafunzo zaidi.
Naye, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Jacob Mkunda amesema JWTZ kwa kushirikiana na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wameandaa mkakati mzuri wa kuboresha na kuifanya JKT kuwa ya kisasa zaidi ili iendane na mabadiliko ya sayansi na teknolojia ulimwenguni.