Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa Watanzania kuwaenzi Mashujaa waliopoteza maisha yao wakiutetea, kuupigania na kulinda Uhuru wa Tanzania kwa kudumisha amani, umoja, mshikamano na kufanya kazi kwa bidii kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania.
Amesema hayo leo wakati akishiriki Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa ambayo kwa mara ya kwanza yamefanyika katika Mji wa Serikali, Mtumba katika Uwanja mpya wa Mashujaa, mkoani Dodoma.
Aidha, Rais Samia amewahimiza Watanzania kutowaruhusu watu au kikundi cha watu wenye nia ovu ya kutaka kuligawa taifa kwa kisingizio chochote kile kwani Tanzania ni moja na haiwezi kugawanyika.
Mbali na hayo, ameielekeza Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na wahusika wote kuendelea kusimamia kwa ukaribu ujenzi wa mnara na uwanja wa Mashujaa ili ukamilike kwa wakati na kwa viwango kama ilivyokusudiwa. Vile vile ameitaka Wizara ya Fedha ihakikishe inatoa fedha kwa kuzingatia mpango kazi wa ujenzi bila kuwepo kwa ucheleweshwaji.
Dkt.Kikwete: Niliuona uwezo wa Rais Samia kiuongozi tangu 2001
Hata hivyo, Rais Samia amekiri kuvutiwa na ramani ya uwanja huo ambao unategemewa kuwa mnara mrefu zaidi Afrika ambapo utakwenda sambamba na shughuli nyingine za kijamii ikiwemo kumbi za mikutano, migahawa ya kimataifa pamoja na vivutio vya watu kupumzika.
“Nimevutiwa sana na ramani ya uwanja wa Mashujaa. Uwanja huu utakuwa na migahawa ya kimataifa, utakuwa na kumbi za mikutano, utakuwa na vivutio vingine vya watu kupumzika na kupata burudani kama michoro ilivyoonesha, kubwa zaidi kutakuwa na mnara mrefu kabisa ndani ya Afrika yetu,” amesema.