Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania inahitaji watendaji kazi wengi zaidi ili kuwahudumia wananchi kutokana na idadi ya watu kuongezeka pamoja na kukua na kufunguka kwa nchi.
Ameyasema hayo Ikulu Chamwino mkoani Dodoma wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi wateule akiwemo Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI, Rogatus Mativila pamoja na viongozi mbalimbali waliopewa hadhi ya Ubalozi.
“Nchi yetu inakua, haikui kwa size, size ni ile ile lakini inakuwa kwa mambo, tumeamua kuifungua, inapofunguka na mambo mengi yanakuja ndani, kwa hiyo wasaidizi wanatakiwa wawe wengi zaidi ili mambo yaende lakini population [idadi ya watu] imekua mno, watu wote hao wanataka huduma, kwa hiyo ni lazima tuhakikishe kila sekta kuna watu wameshika pahali ili kutoa huduma kwa wananchi,” amesema.
Rais Samia atoa onyo kwa wezi wa vifaa miradi ya maendeleo
Aidha, Rais Samia amesema amempa hadhi ya Ubalozi Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Moses Kusiluka ili kumsaidia Rais katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali yanayohitaji uwepo wake pamoja na kuwafikia watu wengi zaidi.
“Katibu Mkuu kiongozi ni msaidizi wa karibu zaidi na Rais, sasa kuna nyakati Rais anazongwa na kazi zingine, na kuna wageni wanaotaka kumwona Rais ambao mtu asiye hadhi ya ubalozi wanakuwa wanyonge kumwona, kwa hiyo tumempa hadhi ya ubalozi Katibu Mkuu Kiongozi ili apate sasa upeo mpana wa kufanya kazi zake, akutane na wengi zaidi,” amefafanua.
Naye Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango amewasihi viongozi walioteuliwa kushirikiana na timu watakazozikuta katika maeneo yao ya kazi wakiwemo Makatibu wakuu na Naibu Makatibu wakuu wao ili kufanikisha utendaji kazi, pamoja mabalozi kufanya kazi zao vyema ili diplomasia ya uchumi iweze kuimarika.