Rais Samia: Tuzo ya CISM ni heshima kwa Watanzania

0
97

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tuzo aliyokabidhiwa na Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani (CISM) ni heshima kwa Watanzania wote na ni msukumo wa kuimarisha michezo ndani ya Majeshi ya Ulinzi na Usalama nchini.

Ameyasema hayo leo Ikulu wakati wa hafla ya kutunukiwa Tuzo hiyo iliyowasilishwa kwake na Makamu wa Rais wa CISM na Mkuu wa Mafunzo ya Ulinzi na Operesheni wa Jeshi la Ulinzi la Nigeria, Meja Jenerali Maikano Abdullahi.

CISM imetoa tuzo hiyo ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wake katika kuliwezesha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kushirikiana kimataifa katika maendeleo ya michezo ya majeshi na kusimamia misingi ya amani, mshikamano, urafiki, usawa, uadilifu na ushupavu.

Rais Samia amesema kuwa majukwaa ya michezo ya kijeshi ni nyenzo muhimu ya kujenga mshikamano wa kijeshi unaovuka mipaka ya kijiografia na tofauti za kimila na kitamaduni, sambamba na kuchochea urafiki na kuaminiana miongoni mwa vikosi vya ulinzi na usalama Barani Afrika.

Send this to a friend