Rais Samia: Uchaguzi CCM ukiimarishe chama kuelekea chaguzi zijazo

0
83

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi, Rais Dkt. Samia Suluhu amewataka wanachama wa chama hicho waliochaguliwa na wanaogombea katika uchaguzi utakaofanyika leo Desemba 7, 2022 jijini Dodoma kutambua kwamba lengo la uchaguzi sio kutafuta ushindi wa mtu mmoja mmoja bali ni mkakati wa kujiimarisha na kujipanga kwa ajili ya kutafuta ushindi wa chama hicho katika chaguzi zijazo.

Ameyasema hayo leo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 10 wa CCM unaondelea jijini Dodoma katika ukumbi wa Jakaya Kikwete ambao umehudhuriwa na wajumbe 1,928 kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar.

“Tuna uchaguzi wa Serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi mkuu wa 2025, wote walioteuliwa kugombea nafasi walizoomba ni washindi kwa sababu chama kimewaamini kuwa yeyote angechaguliwa huku nyuma na leo ni mwanachama thabiti angeongeza nguvu yake kukijenga chama.

“Lakini kwa sababu ya uchache wa nafasi ni vigumu wote kuchaguliwa, kwa kutambua hilo na kupanua wigo wa ushiriki wa wanachama, halmashauri kuu imekuja na mapendekezo katika kufanikisha jukumu lililopo mbele yetu la kutafuta ushindi wa CCM mwaka 2024 na 2025,” amesema.

Makamu wa Rais Argentina ahukumiwa jela miaka sita

Aidha, amesema halmashauri kuu ya chama hicho imepeleka mapendekezo katika mkutano mkuu wa CCM yanayolenga kuongeza nafasi za wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM Taifa kutoka viti 15 Tanzania bara hadi viti 20 hivyo hivyo kwa Zanzibar kutoka 15 hadi 20 pamoja na kuongeza idadi ya wajumbe wa halmashauri ya CCM wanaoteuliwa kutoka wateuliwa saba hadi 10.