Rais Samia: Uchumi wa Tanzania unaimarika

0
45

Rais Samia Suluhu Hassan amesema licha ya hali ya uchumi kushuka wakati anaingia madarakani kutokana na janga la UVIKO 19 kuathiri uchumi wa dunia, kwa sasa uchumi wa Tanzania unaimarika.

Ameyasema hayo wakati akijibu swali katika mdahalo wa wakuu wa nchi uliojadili fursa zilizomo na changamoto zinazozikabili nchi za Afrika uliofanyika Accra, Ghana katika mkutano wa 57 wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Aidha, Rais Samia amesema wakati wa janga la UVIKO 19, uchumi wa nchi ulishuka kutoka asilimia 6.4 hadi asilimia 4 lakini kwa sasa umekuwa na kufikia asilimia 5.2 kwa mwaka huu huku matarajio yakiwa asilimia 6.7 mwaka 2025.

Rais Samia amesema, AfDB na Mashirika ya Kimataifa  yamechangia kuendeleza kilimo, miundombinu ya barabara pamoja na viwanja vya ndege, hivyo kusaidia kuunganisha Tanzania na nchi jirani.

Ameeleza kuwa fedha za UVIKO 19 zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF)  zimesaidia kusambaza maji katika maeneo ya mijini na vijijini ambapo hadi kufikia mwaka 2025 anatarajia usambazaji wa maji maeneo ya vijijini kuwa asilimia 85 na asilimia 95 kwa maeneo ya mijini.

Send this to a friend