Rais Samia: Ulemavu sio kikwazo cha kufanya makubwa

0
38

Rais Samia Suluhu Hassan amesema ulemevu hauzuii kufanya mambo makubwa duniani, bali inapaswa kutayarishwa mazingira, kutoa uwezo wa kuelimisha ili kila mtu aweze kufanya kila kitu.

Amesema hayo leo Desemba 7, 2021 katika hafla iliyofanyika viwanja vya Ikulu Jijini Dar es Salaam kuipongeza Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu kwa Watu wenye Ulemavu (Tembo Warriors) baada ya kufuzu kwenda kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia yatakayo fanyika nchini Uturuki mwaka 2022.

Ametolea mfano washiriki wa mashindano ya urembo kwa wenye ulemavu wa kusikia na watanashati barani Afrika ambao walifanya vizuri na kusema Serikali haitaacha mtu yeyote nyuma katika maendeleo bila kujali hali yake ya maumbile au ulemavu wa viungo.

Rais amewataka wachezaji wa Tembo Warriors kutobweteka na hatua waliyofikia bali waongeze bidii ili wapate ushindi zaidi katika michuano ijayo ya Kombe la Dunia nchini Uturuki.

Ameitaka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuangalia namna bora ya wachezaji wa timu hiyo kukaa pamoja kwa ajili ya maandalizi ya muda mrefu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa katika michuano hiyo ya kombe la dunia.

Send this to a friend