
Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa uamuzi wa kuishirikisha sekta binafsi katika uendeshaji wa bandari umeongeza kwa kiasi kikubwa mapato ya Serikali na kuboresha ufanisi wa utoaji wa huduma.
Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa matanki ya kuhifadhi mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, Rais Samia alisema mapato ya kodi ya forodha yameongezeka kutoka shilingi trilioni 7.3 mwaka wa fedha 2020/21 hadi kufikia trilioni 12.31 mwaka 2023/24.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na mageuzi yaliyofanyika pamoja na ujio na ushiriki wa wawekezaji binafsi, wakiwemo kampuni ya DP World na wadau wengine wanaoendelea kuwekeza katika bandari mbalimbali nchini.
Rais Samia amesisitiza kuwa uamuzi wa kuishirikisha sekta binafsi ulikuwa wa kimkakati na ulihitaji ujasiri mkubwa, lakini umeleta tija kwa kuongeza shehena zinazohudumiwa, kupunguza gharama za uendeshaji na kuharakisha utekelezaji wa mageuzi yaliyokusudiwa.
Aidha, amesema fedha zilizookolewa kupitia upunguzaji wa gharama za uendeshaji sasa zinaelekezwa katika miradi mingine ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa matanki ya kupokea mafuta katika eneo la Kigamboni.
Ameongeza kuwa kasi ya utekelezaji wa mpango mkakati wa kuendeleza bandari imeongezeka maradufu, hatua inayoiwezesha Tanzania kuimarisha ushindani wa bandari zake katika ngazi ya kikanda na kimataifa.







