Rais Samia: Uwekezaji bandarini umezingatia maslahi ya taifa

0
40

Rais Samia Suluhu Hassan amesema uwekezaji utakaofanyika katika bandari ya Dar es Salaam na kampuni ya DP World kutoka Dubai umezingatia maslahi mapana ya nchi na hautoathiri shughuli za kiuchumi.

Ameyasema hayo leo wakati akishiriki halfa ya utiaji saini wa mikataba mahsusi ya uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam Ikulu mkoani Dodoma ambapo amesema lengo la kuruhusu uwekezaji ni kuongeza ufanisi utakaofanya bandari za Tanzania kuwa shindani na bandari nyingine katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.

“Hakuna atakayepoteza kazi, awe mwajiriwa wa bandari au hata wanaofanya kazi zao bandarini, wafanyabiashara walioko bandarini hakuna atakayepoteza kazi, kutakuwa tu na kufuata mfumo flani katika kufanya kazi zetu ili viwango vile vikae sawa tuendane na dunia,” amesema.

Ameongeza kuwa Serikali imefanya uchambuzi wa kina juu ya maoni yaliyotolewa na makundi mbalimbali zikiwemo hoja za wabunge, viongozi wa dini, viongozi wastaafu, vyama vya siasa, asasi za kiraia, wanaharakati huru, vyombo vya habari na maoni ya wananchi kutoka kwenye mitandao ya kijamii na kuyafanyia kazi maoni yote sahihi yaliyotolewa.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka za Bandari Tanzania (TPA), Plasduce Mbossa amesema ufanisi mdogo wa bandari ya Dar es Salaam umetokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa mifumo ya kisasa ya TEHAMA inayoweza kusomana, kutokuwepo kwa maeneo ya kutosha ndani na nje ya bandari kwa ajili ya kuhifadhia shehena za mizigo pamoja na uchache wa magati ambayo yanatumika kama maegesho ya meli.

Send this to a friend