Rais Samia: Vijana wanatoroka kujiunga na vikundi vya ugaidi nje ya nchi

0
44

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na viongozi wa nchi jirani wanaendelea na mazungumzo ili kuona njia bora ya kuwarejesha nchini mwao wakimbizi walioko nchini.

Akihutubia katika Mkutano wa Saba wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF) na Makamanda kwa mwaka 2023 jijini Dar es Salaam, amesema Serikali inafanya mchakato wa kuwachambua wakimbizi hasa kutoka DRC na Burundi ili kuona jinsi ya kuwarudisha.

“Tumefanya kazi hii kwa kiasi kikubwa kwa kushirikiana na lile shirika linaloshughulika na wakimbizi duniani, lakini ukweli ni kwamba lile shirika nalo limeishiwa nguvu kwa hiyo ule moto wa kurudisha wakimbizi kama walivyokuwa wanafanya umepungua,” amesema.

Aidha, amesema kuna matendo ya ugaidi na uharamia pamoja na biashara ya dawa za kulevya ambapo baadhi ya vijana wanashawishiwa na kutoroka nchini na kwenda kujiunga na makundi ya ugaidi nje ya nchi.

“Vijana wetu wanatoroka wanachukuliwa huko wanaingia kwenye vikundi vya ugaidi. Kwahiyo hayo yakitokea inamaana vikundi vile huwezi kusema ni vya Mozambique ni vya DRC, ni vikundi vya Watanzania as long as Watanzania wako mle ndani, hatuwezi kujua lini wanaweza kurudi wakafanyia huku ndani kwetu,” ameeleza.

Mbali na hayo, amelitaka JWTZ kujipanga kuelekea uchaguzi ujao wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu kwa kuwa chaguzi hizo hushirikisha vyama vingi vya siasa na hivyo mambo mengi hutokea.

Send this to a friend