
Rais Samia Suluhu Hassan amesema matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 yalikuwa ni matukio ya kutengenezwa, yakidhamiria kuangusha Dola ya Tanzania.
Ameyaeleza hayo leo Desemba 02, 2025 wakati akizungumza na Wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere (JNICC), akisema vijana wa Kitanzania walifanywa makasuku na kuimbishwa.
“Vijana wetu walifanywa makasuku na kuimbishwa kabisa yaliyotokea Madagascar yatokee na hapa. Lakini ukimvuta kijana pembeni ebu niambie Madagascar kumetokea nini hajui, unataka hapa kitokee nini? Hajui lakini waliimbishwa wimbo huo,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amekaririwa akisema vurugu zile ni mradi mpana wenye nia ovu ulio na wafadhili na watekelezaji. Amesema katika vurugu hizo, wengine waliingia bila ya kujua na kufuata mikumbo huku wengine pia wakijihusisha kwa hadaa za maisha mazuri, na wengine wakilipwa fedha ili kushiriki katika vurugu.
Akionesha kuumizwa na madhara yaliyojitokeza wakati wa matukio hayo, Rais Samia ametaka mjadala wa pamoja, akihoji ikiwa yale yalikuwa maandamano ama vurugu na uharibifu wa mali za umma.








