Rais Samia Suluhu Hassan amesema vyombo vya habari sio mshindani wa Serikali, bali ni mdau na mshiriki muhimu wa shughuli za Serikali, hivyo Serikali haina budi kuweka sera nzuri na kudumisha uhuru wa vyombo vya habari.
Ameyasema hayo wakati wa kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari lililofanyika Jijini Dar es salaam, ambapo Rais Samia ameeleza kuwa yeye ni muumini mzuri wa uhuru wa Vyombo vya Habari, hivyo Serikali inaendelea kushughulikia kero za muda mrefu zilizokuwa zikiikabili sekta ya Habari nchini.
“Huko nyuma kipindi fulani vyombo vya habari na Serikali vilikuwa vinavutana, wao wamevuta na sisi tumevuta lakini tuliona hatutofika pahala hivyo tuliamua kukaa sehemu moja na kufanya kazi kwa pamoja,” amesema.
Aidha, Rais Samia amewaasa wandishi wa Habari kutumia uhuru wa vyombo vya Habari kwa weledi, kwa kuzingatia dhana ya uandishi wa Habari pamoja na kuwa wazalendo kwa kuripoti Habari zenye tija kwa nchi na si kulichafua taifa.
Mbali na hayo, Rais Samia ameagiza Wizara na Taasisi za Umma zote zinazodaiwa na vyombo vya habari zihakiki madeni ya vyombo hivyo na kulipa madeni yote yanayolipika kabla ya Januari 2025.