
Rais Samia Suluhu Hassan ameielekeza Ofisi ya Mashtaka kuwafutia makosa vijana walioonekana kushiriki vurugu siku ya uchaguzi, Oktoba 29, 2025 kwa kufuata mkumbo bila kuelewa madhara ya kitendo hicho.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bunge la 13 jijini Dodoma, Rais Samia amesema video mbalimbali za vurugu zinaonesha kuwa baadhi ya vijana walijiingiza kwenye vitendo vya kihalifu kwa ushabiki tu, hivyo ni muhimu kuchuja makosa yao ili kutenda haki.
“Kuna wakati vijana hufuata mkumbo wa uhalifu kwa ushabiki. Ninatambua kwamba vijana wengi waliokamatwa na kushitakiwa kwa makosa ya uhaini hawakujua wanachokifanya. Nikiwa mama na mlezi wa Taifa hili, ninavielekeza vyombo vya sheria, na hasa Mkurugenzi wa Mashtaka kuangalia kiwango cha makosa yaliyofanywa na vijana wetu,” ameelekeza Rais.
Ameongeza kuwa, “Kwa wale ambao wanaonekana walifuata mkumbo na hawakudhamiria kufanya uhalifu, wafutiwe makosa yao.”
Akinukuu Kitabu cha Luka 23:34, Rais Samia amesema msamaha huo unaendana na mafundisho ya dini, akisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kulinda mustakabali wa vijana na kudumisha amani ya nchi.
Aidha, amesema nchi inapoelekea kwenye maelewano na amani, ameunda tume ya uchunguzi ambayo itabainisha chanzo cha vurugu hizo.








