Rais Samia: Waliozusha miradi haitaendelezwa hawakutumia hekima

0
49

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewakosoa wale wote wanaosema kuwa asingeweza kukamilisha miradi iliyoachwa awamu ya tano chini ya Hayati John Pombe Magufuli na kusema kuwa miradi hiyo imeanzishwa chini ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi akiwa Makamu wa Rais, hivyo yeye ni sehemu ya miradi hiyo.

Rais Samia ameyasema hayo leo alipokuwa akizindua nyumba 644 za makazi Magomeni Kota mkoani Dar es Salaam na kueleza kuwa hakuna sababu ya miradi hiyo kutoendelezwa kwa kuwa tayari ipo katika ilani ya chama, na miradi yote mikubwa iliyoachwa na Hayati Magufuli itaendelezwa.

“Kwa kunitazama sura na kusema asingeweza kutekeleza miradi, nadhani hekima haikutumika, lakini tuwaombee na sisi tujiombee Mungu atupe uwezo zaidi, hekima zaidi tuweze kuendeleza miradi hii kwa maendeleo ya nchi yetu,” amesema.

Aidha, Rais Samia amefurahishwa na usanifu na ujenzi wa magorofa uliofanywa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) chini ya usimamizi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi huku akiwataka kushirikiana na na sekta binafsi ili kuendeleza ujenzi wa nyumba zote katika maeneo yote yaliyo wazi.

Ameridhia ombi la kutoa muda wa miezi mitatu kwa wananchi kukaa kwenye nyumba hizo bure kwa miezi mitatu, na baada ya hapo wataanza kulipia gharama za uendeshaji.

Mwisho amewataka wakazi watakaopenda kuishi katika nyumba hizo kuanza kulipia kidogo kidogo kuanzia sasa pia kujali usafi na kushirikiana pindi watakapoanza kuishi katika nyumba hizo.

Send this to a friend