Rais Samia: Watanzania changamkieni fursa za ukuaji wa Kiswahili duniani

0
77

Rais Samia Suluhu Hassan amewahakikishia Watanzania kuwa serikali imeweka mikakati ya kuhamasisha Watanzania wenye ueledi katika lugha ya Kiswahili kuchangamkia fursa zitokanazo na kukua kwa lugha hiyo katika mataifa mbalimbali duniani.

Ameyasema hayo Julai 7 kupitia hotuba fupi ya maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani ambapo katika hotuba yake amependekeza kaulimbiu ya mwaka huu 2023 isomeke kuwa ‘Kiswahili ni zaidi ya Lugha’.

“Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeweka mikakati ya kuhamasisha watanzania wenye ueledi katika lugha ya Kiswahili kuchangamkia fursa zitokanazo na kukua kwa lugha kama vile ukalimani, tafsiri, uhariri, uandishi wa habari, uandishi wa vitabu, utangazaji na ufundishaji wa Kiswahili kwa wageni na hata utungaji na muziki,” ameeleza.

Aidha, Rais Samia amesema Tanzania inafarijika kuwa na umoja na mshikamano unaochangiwa na kuwa na lugha ya kitaifa inayounganisha na kuleta amani na utulivu vinavyowawezesha kujenga taifa kiuchumi, kijamii, kisiasa na kitamaduni.

Ameongeza kuwa Tanzania kama kitovu cha lugha ya Kiswahili, Watanzania hawana budi kukipa nguvu na kuongeza matumizi yake katika nyanja za kiuchumi, kidiplomasia, sayansi na teknolojia.

Send this to a friend