Rais Samia Suluhu Hassan ametoa wito kwa wazazi kuwajibika katika malezi ya watoto wao kwa kufuata maadili mema ili kuokoa kizazi kilichopo na kwa maendeleo ya nchi.
Ameyasema hayo leo katika akihutubia Baraza la Eid el-Fitr lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
“Kuna usasa natambua na tunaona ndio maendeleo na ustaarabu, lakini tutapata maendeleo makubwa zaidi na ustaarabu makubwa zaidi tutakapokwenda na usasa zaidi kwa kuendana na tamaduni zetu.
Kwa hiyo niwaombe sana wazazi wenzangu tusikwepe majukumu, twende tukatunze watoto wetu vile sisi tulivyotunzwa. Sisi tulitunzwa leo tunaitwa bibi tunaitwa mama, sasa sijui tunatetereka wapi kutunza wale wanaotuita bibi, wanaotuita mama,” amesema.
Aidha, Rais Samia amewasihi akina mama kuwa mstari wa mbele katika kuwadhibiti watoto wao na kuacha kuitegemea Serikali kufanya hivyo ili kulinda maadili ya watoto juu ya tamaduni zisizofaa.
Katika hotuba hiyo, amewapongeza waumini wa dini ya Kiislamu na Wakristo kwa ushirikiano wao katika kipindi cha Kwaresma na Ramadhan na kufanya fungo zote kuwa njema na kumalizika kwa amani.