Rais Samia: Waziri Mkenda alitoroka, hakuniaga
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameitembelea Shule ya Sekondari Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam na kuzungumza na wanafunzi pamoja na walimu wa shule hiyo.
Akizungumza na wanafunzi hao, Rais Samia ametoa majibu ya maombi ya shule hiyo yaliyotolewa katika sherehe ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa kwa Rais Samia iliyofanyika shuleni hapo huku mgeni Rasmi akiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.
Aidha, amesema kuwa ingawa Waziri huyo alifanya makosa na kuhudhuria kwenye tukio hilo bila ya kumpa taarifa, aliyapokea maombi yaliyotolewa na shule hiyo na kumwambia kuwa atafute wenzake wagawane majukumu na kuyatekeleza kwa kuwa ni jukumu lake.
“Natambua mliwasilisha maombi maalumu kupitia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknoloji, Prof. Mkenda ambaye siku ile alikuwa mgeni rasmi, Lakini alifanya dhambi, alipokuja huku hakuniaga aliamua kunishtukiza lakini mlimpa maombi yenu na aliyafikisha kwangu,” amesema Rais Samia
Hata hivyo amemtaka Prof. Mkenda kuwa pindi wanapojenga hosteli za wanafunzi hao wajenga na nyumba za wasimamizi wa wanafunzi hao ili wawe karibu na wanafunzi.
Rais Samia amewaahidi kutekeleza maombi yaliyotolewa kwa kadri serikali itakavyoweza ikiwa ni pamoja na ujenzi wa maktaba, vyumba vya madarasa, gari la dharura na nyasi bandia kwa shule hiyo pamoja na shule mbili zilizoko Jirani
Mbali na hayo Rais Samia amekubali ombi la mwanafunzi Emmanuel Mzena la kumsomesha na kumfungulia taasisi maalumu ili kuwasemea watoto waliofichwa na kukosa elimu.