Rais Samia Suluhu Hassan amesema baada ya Serikali kutatua tatizo la kisheria kuhusu mradi wa Same – Mwanga, kwa sasa Serikali inatafuta namna ya kutatua tatizo la upatikanaji fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huo ili kufikia mwakani uwe umekamilika.
Ameyasema hayo wakati akishuhudia utiaji saini wa mikataba ya mradi wa maji wa miji 28 leo katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma na kusema kuwa, Serikali itaendelea kujenga miradi ya maji katika kila eneo la nchi ili kufikia 2025 huduma ya maji safi na salama ifikie asilimia 85 vijijini na asilimia 95 mijini.
“Kuna dalili zote kwamba tutaweza kwasababu mpaka leo tulipo kwa vijijini tumeshafanya asilimia 74, lakini miradi 1,000 inayoendelea vijijini Tanzania nzima itakwenda kuchangia asilimia 4, kwa hiyo mpaka Juni mwakani tutakuwa tumefika asilimia 78. Tuna miaka mingine miwili ya utaekelezaji wa miradi ya maji ambayo itatusogeza kufikia asilimia 85,” amesema.
Aidha, ameipongeza Wizara ya Maji kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhakikisha wanatekeleza miradi ya maji nchini pamoja na kubana matumizi katika miradi inayotekelezwa kwa sasa.
“Ni kweli kuwa Wizara ya Maji mmebadilika sana, mlinipa tabu mwanzo, tulielezana ukweli, mko kwenye mstari, sasa tunakwenda vizuri” amesema.
Mbali na hayo, ameishukuru Serikali ya India kupitia Benki ya Exim kwa kutoa mkopo wa TZS trilioni 1.2 ambao utakwenda katika kutekeleza miradi ya maji katika miji 28.