
Rais Donald Trump amesema ana hasira sana na amechukizwa na Rais wa Urusi, Vladimir Putin kukosoa uhalali wa uongozi wa Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine, akiongeza kuwa kauli hizo hazina mustakabali mzuri.
Hivi karibuni Putin alisema serikali ya mpito ianzishwe nchini Ukraine, ambayo ingeweza kumlazimisha Zelenskyy kuondoka madarakani.
Aidha, Trump ametishia kutoza ushuru wa asilimia 50 kwa nchi zinazonunua mafuta ya Urusi ikiwa Putin hatakubali kusitishwa kwa mapigano.
“Ikiwa mimi na Urusi hatuwezi kufikia makubaliano ya kusitisha umwagaji damu nchini Ukraine, na ikiwa nitadhani kuwa ni kosa la Urusi, nitaweka ushuru kwenye mafuta, kwenye mafuta yote yanayotoka Urusi.
“Hiyo itakuwa kama unanunua mafuta kutoka Urusi, hutafanya biashara Marekani. Kutakuwa na ushuru wa asilimia 25 hadi 50 kwenye mafuta yote,” amesema.