Rais wa Marekani, Donald Trump ametia saini amri inayoiwekea vikwazo Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), akiituhumu kwa vitendo vinavyokiuka sheria na visivyo na msingi vinavyoilenga Marekani na mshirika wake wa karibu, Israel.
Hatua hiyo imekuja baada ya mahakama hiyo kutoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na Waziri wa zamani wa Ulinzi, Yoav Gallant.
Amri hiyo inaweka vikwazo vikali kwa maafisa wa ICC na familia zao, ikiwa ni pamoja na kuzuiwa kwa mali zao na marufuku ya kuingia Marekani. Trump anadai kuwa ICC haina mamlaka juu ya Marekani na Israel, na kwamba hatua zake zinaweka hatarini usalama wa taifa na sera za kigeni za Marekani.
“Tabia hii mbovu inatishia kukiuka uhuru wa Marekani na inadhoofisha kazi muhimu ya usalama wa kitaifa na sera ya kigeni ya serikali ya Marekani na washirika wetu, ikiwa ni pamoja na Israel,” imesema amri hiyo.
Novemba mwaka jana, ICC ilitoa hati ya kukamatwa kwa Netanyahu kwa tuhuma za uhalifu wa kivita huko Gaza, jambo ambalo Israel inakanusha, pia ICC ilitoa kibali cha kukamatwa kwa kamanda wa Hamas.