Rais: Tumeanza kuifufua bandari ya Tanga ili vijana wapate ajira

0
25

Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imeanza kuuifufua bandari ya Tanga ili kuongeza uzalishaji wa ajira kwa vijana hususan kwa wakazi wa mkoa huo.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi ikiwa ni sehemu ya ziara yake mkoani humo ambapo amesema tayari kiwango cha mizigo kwenye bandari hiyo kimeongezeka kutoka tani laki nne hadi tani milioni 1.2 akiongeza kuwa mipango ya serikali ya baadaye ni kuifanya bandari hiyo kuwa maalum kwa mbolea na mazao ya chakula.

Aidha, Rais Samia ameiagiza Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kupitia vipengele vya mikataba ya ubinafsishwaji wa viwanda na mashamba ya serikali mkoani Tanga ili kubainisha kama mienendo ya wawekezaji haivunji masharti ya mikataba yao.

“Nimetoa agizo kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ipitie vipengele vyote vya mikataba ya ubinafsishwaji na kubainisha endapo mienendo ya wawekezaji hao haivunji masharti ya mikataba yao, na kama wamevunja watushauri hatua zitakazotakiwa kuchukuliwa kwa mujibu wa mikataba husika ili mashamba hayo, viwanja vilivyobinafsishwa na havifanyi kazi tuweze kuchukua hatua nyingine ili ajira zitengenezwe,” amesema.

Mbali na hayo, Rais Samia amesema matamanio yake ni kuirudisha Tanga ya viwanda kama ilivyokuwa hapo nyuma, na kwamba serikali tayari imeanza kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kufanya utanuzi wa viwanda na kujenga viwanda ili kuzalisha ajira.

Send this to a friend