Rais: Tutapitia upya maslahi ya Kada ya Ualimu ili kuipa hadhi stahiki

0
3

Rais Samia Suluhu Hassan amesema ili kuendana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, toleo la 2023, Serikali itapitia upya maslahi ya kada ya Ualimu ili kuipa hadhi inayostahiki kada hiyo.

Amesema hayo katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, toleo la 2023 ambapo ameeleza kuwa sambamba na hilo serikali itaendelea kuajiri walimu wenye sifa na kuwapa mafunzo stahiki.

“Serikali itaendelea kuajiri walimu wenye sifa na kuwapa mafunzo stahiki ili waendane na mwelekeo wa sera hii. Aidha tutapitia upya maslahi ya kada ya ualimu nchini ili kuipa hadhi inayostahiki kama mama wa taaluma zote duniani,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amesema dhamira ya Serikali ni kuwaandaa vijana wanaojiamini na wenye nyenzo stahiki za kukabiliana na ushindani wa Kikanda na Kimataifa, ili kwa kutumia utajiri wa rasiliamali za nchi waweze kunufaika kiuchumi.

Ameongeza kuwa wakati taifa linaelekea kukamilisha Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050, kwa upande wa elimu shabaha ya serikali ni kujenga jamii iliyoerevuka na iliyopata ujuzi unaoendana na mahitaji ya wakati na ujuzi utakaowezesha kukabiliana na soko la ajira.

Send this to a friend