Rais Samia Suluhu amesema Serikali itaunda kamati itakayoshirikisha wajumbe kutoka serikalini na sekta binafsi ili kupitia kwa undani mfumo mzima wa kodi na kuondoa changamoto zinazolalamikiwa na wafanyabiashara.
Ameyasema hayo leo katika mkutano wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) Ikulu, Dar es Salaam ambapo amesema kamati hiyo itakuwa na kazi ya kupitia kwa undani na kuwasilisha mapendekezo na ushauri utakaofaa kwa nchi.
“Kabla ya kikao hiki, niliita baadhi ya wafanyabiashara juzi tarehe 27, nikakaa na kusikiliza kuna nini upande wenu, na suala la kodi lilijitokeza kama ndilo suala kubwa kuliko yote. Katika kushauriana na serikali yangu, tumekubaliana pamoja na kamati zenu za TNBC, lakini serikali tutakwenda kuunda kamati itakayopitia mfumo mzima kuanzia sera na sheria jinsi zinavyotekelezwa,” amesema.
Aidha, katika kuongeza chachu ya kukuza biashara na nchi jirani, Rais Samia Suluhu amewaagiza wakuu wa Mikoa na Wilaya za mipakani kuhakikisha kuwa biashara mipakani zinafanyika kwa wepesi kwa kuondoa vikwazo na vizuizi visivyo vya lazima.
Mbali na hayo, Rais Samia ameziagiza Balozi za Tanzania katika maeneo mbalimbali kuendelea kusaidia wadau wa sekta binafsi hususan makampuni ya Tanzania kuchangamkia fursa zinazopatikana katika maeneo hayo, pamoja na kuzihamasisha sekta binafsi nchini kushirikiana na serikali kuwekeza katika Miradi ya Ubia (PPP).