Rais: Uanzishwaji wa Benki ya Ushirika Tanzania ni utekelezaji wa wazo la muda mrefu

0
3

Rais Samia Suluhu Hassan amesema uanzishwaji wa Benki ya Ushirika Tanzania ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na utekelezaji wa wazo la muda mrefu la kuhakikisha sekta ya ushirika inakuwa na benki kubwa inayoihudumia.

Rais Samia ameyasema hayo leo wakati akizindua Benki ya Ushirika Tanzania, katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Benki hiyo itakayojikita kuchochea ufadhili wa mitaji zaidi kwenye sekta ya ushirika, inamilikiwa kwa asilimia 51 na vyama vya ushirika, asilimia 20 na Benki ya CRDB, asilimia 10 na Serikali na asilimia 9 ni wanahisa wengine.

“Ni jambo la furaha na matumaini kuona benki hii haijaanza kinyonge, inazinduliwa leo ikiwa na mtaji wa shilingi bilioni 58. Kiasi hiki kitachangia kuimarisha upatikanaji wa mitaji ili kuongeza tija kwa kilimo na kuhakikisha usalama wa chakula na kuchochea maendeleo vijijini,” amesema.

Aidha, Mhe. Rais Dkt. Samia amebainisha kuwa dhamira ya Serikali ni kuona ushirika unaimarika na kuongeza mchango wake kwenye Pato la Taifa na kukuza uchumi wa nchi kwa ujumla.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amezitaka Wizara ya Fedha, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutafuta jawabu la changamoto ya upatikanaji mitaji katika sekta ya kilimo nchini.

Send this to a friend