Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye kukagua ujenzi wa SGR, Dar es Salaam

0
56

 

Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye anatarajiwa kutembelea Bandari ya Dar es Salaam na kukagua ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) unaoendelea nchini kutokea stesheni ya Dar es salaam hadi stesheni ya Kwala – Ruvu mkoani Pwani pamoja na kutembelea bandari kavu ya Kwala inayojengwa na Mamlaka ya Bandari Tanzania katika eneo hilo ili kujionea maendeleo ya ujenzi.

Rais Ndayisimiye atafanya hilo ikiwa ni siku yake ya pili ya zaira nchini ambapo anatarajiwa kuwasili Oktoba 22, 2021 kwa ajili ya zaiara ya kikazi ya siku tatu.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema Rais Ndayishimiye atawasili katika uwanja wa ndege wa Dodoma Oktoba 22 na kuelekea Ikulu ya Chamwino ambako atapokelewa rasmi na mwenyeji wake, Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Akiwa Ikulu Chamwino pamoja na mambo mengine atakagua gwaride la heshima na kupigiwa mizinga 21 kwa heshima yake na baadaye viongozi hao watakuwa na mazungumzo ya faragha na kufuatiwa na mazungumzo rasmi.

Balozi Mulamula amesema akiwa jijini Dodoma Oktoba 22 Rais Ndayishimiye atatembelea na kuweka jiwe la msingi katika kiwanda cha kuzalisha mbolea ya asili yenye mchanganyiko wa madini ya phosphate na samadi kinachojengwa katika eneo la viwanda la Nala, kiwanda ambacho kinajengwa na wawekezaji wa kampuni ya Itracom Fertilizers Limited (ITRACOM) kutoka nchini Burundi na baadaye jioni atahudhuria dhifa ya kitaifa itakayofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma.

Balozi Mulamula ameongeza kuwa Oktoba 23, 2021 Rais Ndayishimiye ataelekea Zanzibar ambako atapokelewa na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi na kuwa na mazungumzo na mwenyeji wake huyo. Baada ya hapo ataelelekea mkoani Dar es Salaam ambapo ataungana na mwenyeji wake Rais Samia Suluhu Hassan.

Send this to a friend