![](https://swahilitimes.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/gustavo-petro-a-une-idee-pour-stopper-le-trafic-de-cocaine-sa-legalisation-photo-sipa-sebastian-barros-1738831270-905x613.jpg)
Rais wa Colombia, Gustavo Petro, amesema biashara ya kokeini inaweza kudhibitiwa kwa urahisi ikiwa dawa hiyo itahalalishwa duniani kote, kwakuwa dawa hiyo si mbaya zaidi kuliko whisky.
Katika mkutano wa mawaziri uliorushwa moja kwa moja, Petro amesema Kokeini ni haramu kwa sababu inatengenezwa Amerika ya Kusini, si kwa sababu ni mbaya zaidi kuliko whisky, akiongeza kuwa wanasayansi wamechambua suala hilo.
Kiongozi huyo aliyeingia madarakani mwaka 2022, ameahidi kupambana na biashara ya dawa za kulevya na kudhibiti matumizi ya dawa haramu. Hata hivyo, tangu aingie madarakani, uzalishaji wa kokeini nchini Colombia umeongezeka.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC), kilimo cha majani ya coca nchini Colombia kiliongezeka kwa asilimia 10 mwaka 2023 ikilinganishwa na mwaka uliopita, huku uzalishaji wa kokeini ukifikia tani zaidi ya 2,600, ongezeko la asilimia 53.
Colombia ni mzalishaji mkuu wa kokeini duniani, hasa kwa soko la Marekani na Ulaya, na serikali imekuwa ikipambana na biashara ya dawa za kulevya kwa miongo kadhaa.