
Mahakama ya Katiba ya Korea Kusini imethibitisha kuondolewa madarakani kwa Rais Yoon Suk Yeol, ambaye alipigiwa kura ya kuondolewa na wabunge mwezi Desemba, 2024 baada ya kutangaza sheria ya kijeshi.
Akitoa hukumu, Jaji amesema hatua ya Yoon kutangaza agizo la kijeshi iliharibu haki za kimsingi za kisiasa za raia, na kwamba ilikiuka kanuni za utawala wa sheria na demokrasia.
Uamuzi wake wa kupeleka majeshi mitaani ulisababisha mgogoro mkubwa wa kisiasa ambao haujawahi kushuhudiwa nchini humo kwa kipindi cha miongo kadhaa.
Maelfu ya watu waliomuunga mkono na waliompinga walikusanyika katikati ya jiji la Seoul wakisubiri uamuzi huo, na wakosoaji wake walishangilia kwa furaha baada ya hukumu hiyo kutolewa alfajiri ya Ijumaa.
Nchi hiyo sasa ina siku 60 kufanya uchaguzi wa haraka kupata kiongozi atakayechukua nafasi yake.