Rais wa Malawi azuia yeye na baraza la mawaziri kusafiri nje ya nchi

0
55

Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera amechukua hatua kali za kubana matumizi kwa kusitisha mara moja safari zake zote za kimataifa na serikali yake, akilenga kuhifadhi fedha kutokana na hali mbaya ya uchumi nchini humo.

Hatua hiyo imekuja baada ya sarafu ya Malawi kuporomoka kufuatia kupokea mkopo wa dola milioni 174 [TZS bilioni 434.6] kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ili kufufua uchumi uliokuwa hatarini.

Rais Chakwera pia ameagiza mawaziri wote walioko nje ya nchi kurudi nyumbani pamoja na kuondoa ruzuku ya mafuta kwa maafisa wa serikali kwa asilimia 50 ikiwa na lengo la kukabiliana na gharama ya maisha nchini humo, ambao umesababisha upungufu wa petroli na dizeli pamoja na mfumuko wa bei.

Katika hotuba iliyotangazwa kwenye televisheni, Rais Chakwera alisema uamuzi huo utadumu hadi mwisho wa mwaka wa fedha mwezi Machi 2024 huku akiahidi pia kupunguza mzigo wa kodi kwa watu binafsi na kuongeza mishahara ya watumishi wa umma katika bajeti ijayo.

IMF imethibitisha mkopo wa miaka minne wa dola milioni 174, siku chache baada ya benki kuu ya Malawi kutangaza kushusha thamani ya sarafu yake kwa asilimia 44.

Hata hivyo, wachambuzi wanahofia kuwa hatua hiyo inaweza kusababisha kuongezeka kwa bei na kuzorotesha zaidi hali ya kifedha kwa wananchi wa Malawi.

Send this to a friend