Rais wa Marekani, Joe Biden amepongeza uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) wa kutoa hati ya kukamatwa kwa Rais wa Urusi, Vladimir Putin.
Mahakama ya ICC inamtuhumu Rais Putin kwa kufanya uhalifu wa kivita nchini Ukraine jambo ambalo Rais Biden amesema kiongozi huyo amefanya uhalifu wa kivita wa wazi.
Rais Putin anadaiwa kufanya uhamishaji haramu wa watoto kutoka Ukraine hadi Urusi tangu uvamizi wa Moscow nchini humo mwaka 2022, madai ambayo Moscow imeyapinga vikali.
ICC yatoa hati ya kukamatwa Rais Vladimir Putin
Umoja wa Mataifa (UN) pia ulitoa ripoti mapema wiki hii ambayo iligundua kitendo cha Moscow kuwaondoa watoto wa Ukraine kwa lazima na kuwapeleka katika maeneo yaliyo chini yao, jambo linalohalalisha kuwa ni uhalifu wa kivita.
Katika taarifa iliyotolewa siku ya Ijumaa Machi 17, 2023, ICC imesema ina sababu za kuamini kuwa Putin alitenda uhalifu huo moja kwa moja pamoja na kufanya kazi na wengine.