Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Felipe Jacinto Nyusi anatarajia kuanza ziara nchini Tanzania kuanzia Julai 1 hadi Julai 04, 2024 kufuatia mwaliko kutoka kwa Rais Samia Suluhu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba (Mb.) amesema ziara hiyo inalenga kuimarisha zaidi uhusiano pamoja na kukuza ushirikiano wa kiuchumi kati ya mataifa hayo mawili.
“Ziara hii itawapa fursa viongozi wetu kujadili namna ya kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya mataifa yetu mawili, hususani katika nyanja za biashara na uwekezaji, kilimo, madini, utalii pamoja na mafuta na gesi. Kama mnavyofahamu, mataifa yetu mawili yana utajiri mkubwa wa maliasili, ikiwemo mafuta na gesi,” amesema.
Amesema baada ya mapokezi Rais Samia na mgeni wake watafanya mazungumzo ya faragha na kufuatiwa na mazungumzo rasmi ikiwa ni pamoja na kushuhudia uwekaji saini wa mikataba mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi hizo na baada ya hapo watazungumza na waandishi wa habari.
Aidha, amesema Julai 03, Rais Nyusi atakuwa mgeni rasmi katika hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam, maarufu Sabasaba, na kisha kuelekea Zanzibar kwa ziara binafsi kabla ya kurejea nchini Msumbiji Julai 4.
“Kama mnavyofahamu, Tanzania na Msumbiji zina uhusiano mzuri, uhusiano wetu ni wa kihistoria na kidugu. Baadhi yetu mnafahamu kuwa chama Tawala cha FRELIMO kilizaliwa hapa nchini kwetu, na kiongozi wake wa kwanza alikuwa Hayati Eduardo Chivambo Mondlane, aliyeuawa hapa Dar es Salaam mwaka 1969,” ameeleza.