Rais wa Sri Lanka akimbia nchi
Rais wa Sri Lanka, Gotabaya Rajapaksa amekimbia nchi kwa ndege ya kijeshi huku maandamano makubwa yakiendelea nchini kwake kuhusu mdororo wa kiuchumi.
Taarifa ya kuondoka kwake imethibitishwa na Jeshi la anga la nchi hiyo, na kwamba amesafiri kwa ndege hadi Maldives akiwa na mkewe na maafisa wawili wa usalama.
Kaka yake Rajapaksa, Waziri wa zamani wa Fedha, Basil Rajapaksa pia ameondoka Sri Lanka na inasemekana anaelekea nchini Marekani.
Watakaosoma Kiswahili vyuoni kupewa kipaumbele kwenye mkopo
Aidha, inadaiwa Rais Rajapaksa alitaka kukimbia nchi kabla ya kujiuzulu ili kusiwe na uwezekano wa kukamatwa, huku ripoti zikisema kuna uwezekano mkubwa kwa Rais huyo kukimbilia nchi nyingine barani Asia.
Baadhi ya waandamanaji wamekasirishwa na kuondoka kwake, wakimtaka kuwajibika kwa tuhuma zinazomkabili.
“Tunataka kumbakisha, tunataka pesa zetu zirudishwe na tunataka kuwaweka Rajapaksa wote katika gereza la wazi ambapo wanaweza kufanya kazi za shamba,” amesema mwandamanaji.
Rais Rajapaksa alikuwa mafichoni baada ya umati wa watu kuvamia makazi yake siku ya Jumamosi na kuahidi kujiuzulu Jumatano Julai 13.