Rais wa Zambia aongoza maomboleza kifo cha samaki

0
43

Rais wa Zambia, Edgar Lungu ameungana na wananchi hasa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Copperbelt (CBU) kuomboleza kifo cha samaki aliyeaminika kuwa na bahati.

Wanafunzi wa CBU wamewasha mishumaa na kuzunguka katika kampasi ya chuo hicho kuomboleza kifo cha samaki huyo aliyekua akitunzwa katika ziwa chuoni hapo.

Kupitia ukurasa wake wa Facebook Rais Lungu amemnukuu mwanaharakati Mahtma Gandhi kuwa maendeleo na maadili ya taifa yanathibitika pia namna linavyowatunza wanyama.

Kwa miongo miwili wanafunzi wa CBU walikuwa wakiamini samaki huyo aliyefahamika kwa jina la Mafishi (samaki mkubwa kwa lugha ya Kibemba) alikuwa akiwaletea bahati nzuri kwenye mitihani.

Baadhi ya wanafunzi walikuwa wanakwenda kumuona samaki hiyo kabla ya mitihani wakiamini atawasaidia huku wengine wakiamini amekuwa akiwasaidia kuondoa msongo wa mawazo.

Mafishi anakadiriwa kuwa na miaka 22 na ametunzwa chuoni hapo zaidi ya miaka 20 . Uongozi wa chuo umesema uchunguzi wa kifo hicho unaendelea.

Send this to a friend