Rais wa Zimbabwe aapa kuwashughulikia wapinzani na wanaharakati
Sintofahamu umeendelea kutawala nchini Zimbabwe huku pande mbalimbali zikirudhiana lawama ambPo Rais Emmerson Mnangagwa ameshutumu vyama vya upinzani na nchi za kigeni kwa kutekeleza uchonganishi, huku watetezi wa haki za binadamu wakishutumu vyombo vya dola kwa kuwazuia kutenda kazi yao.
Wakati hali hiyo ikiendelea kutamalaki, Rais Mnangagwa ameapa kupambana vikali na wapinzani na wanaharakati wa haki za binadamu baada ya kuongezeka kwa maandamano ya kupinga vitendo vya rushwa na kutoridhishwa na namna hali ya uchumi inavyoshughulikiwa nchini humo.
Serikali imesema kuwa kudorora kwa uchumi wa nchi hiyo kumechangiwa kwa kiasi kikubwa na vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na nchi za magharibi.
”Wale wanaochochea chuki na kuvunja umoja hawatashinda. Watu ambao wamejaribu kuwagawa watu wetu na kudhoofisha mifumo yetu watashughulikiwa,” amesema kiongozi huyo alipozungumza kwa njia ya televisheni mapema leo.
Wiki iliyopita wanaharakati na vyama vya upinzani viliiitisha maandamano nchini humo, lakini vyombo vya ulinzi viliwataka wananchi kutoitikia wito huo, badala yake wakae majumbani mwao.