Rais: Wapuuzeni wenye chokochoko, watavuruga amani

0
42

Rais Samia Suluhu Hassan amewasihi wakazi wa mkoa wa Morogoro pamoja na wananchi wengine kuendelea kuitunza amani iliyopo nchini kwasababu ndio msingi mkuu wa maendeleo ya taifa lolote duniani.

“Kuna baadhi ya watu wameshaanza chokochoko naomba muwapuuze kwani hawawatakii mema, wanataka kuvunja amani ya nchi iliyopo kwa muda mrefu na kusababisha vurugu nchini,” amesema Rais Samia

Amesema hayo leo mara alipowasili mkoani Morogoro katika ziara ya kikazi ya siku mbili.

Aidha, amewapongeza wakazi wa mkoa huo kwa kuwa sehemu ya miradi mikubwa miwili ya kimkakati ya Reli ya Kisasa (SGR) na Mradi wa Kufua Umeme wa Mwalimu Nyerere katika mto Rufiji.

Amesema kutokana na kuwepo kwa miradi hiyo mkoani Morogoro ni vyema wananchi wakawa walinzi ili iweze kuwanufaisha wao na taifa kwa ujumla.

Akiwa katika eneo la Kibaigwa mkoani Dodoma njiani kuelekea mkoani Morogoro, Rais Samia amewataka wananchi wa eneo hilo na Watanzania kwa ujumla kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Corona kwa kufuata maelekezo ya wataalam wa Afya ili kuepuka kupata maambuzi ya ugonjwa huo.

Send this to a friend