RC aamuru walimu waliogomea uhamisho kuripoti haraka kazini

0
60

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha amewaamuru walimu wawili wa shule ya Msingi ya Mabatini, iliyopo Manispaa ya Tabora, Juma Mahundi na Rose Mgaya, waliogoma kuripoti katika vituo vyao vipya vya kazi waripoti haraka iwezekanavyo.

Taarifa zinaeleza kuwa walimu hao walipatiwa uhamisho Mei 06, mwaka huu ambapo Mwalimu Rose Mgaya, alihamishiwa katika Shule ya Msingi ya Farm Nyamwezi na Mwalimu Juma Mahundi alihamishiwa katika Shule ya Msingi ya Ndevelwa, zote zilizopo ndani ya Manispaa ya Tabora.

Akizungumza katika kikao na walimu hao, Mkuu wa Mkoa amewataka walimu hao kuripoti kabla Serikali haijawachukulia hatua za kisheria.

“Mamlaka ikiamua toka hapa hamia sehemu fulani vinginevyo kuna matatizo ya kiafya kila mmoja anajua na hakuna ubishi katika hilo, lakini huwezi kukataa [uhamisho] kwa ubavu kwa sababu una ndugu na jamaa,” ameeleza.

Aidha, mkuu wa mkoa amesema serikali haitaendelea kuwavumilia watumishi wanaochagua mazingira ya kazi na kudumaza juhudi za serikali katika kutoa elimu bora kwa wanafunzi wa maeneo ya pembezoni.