Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameitaka Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) kuangalia namna ya kuongeza muda wa kufanya kazi hadi kufikia saa 24 badala ya muda uliopo sasa.
Ametoa kauli hiyo wakati akizindua safari za mabasi hayo kati ya Gerezani hadi Mbagala Rangi Tatu ambayo imelenga kurahisisha huduma ya usafiri kwa watu wanaotaka kutembelea maonesho ya Sabasaba yanayotarajia kuanza kesho Julai 28, 2023.
“Moja ya jambo ambalo sifurahishwi ni DART kufanya kazi kwa saa kadhaa nataka ikiwezekana wafanye kazi kwa saa 24, kama mtu ametoka saa saba usiku akute basi,” amesema.
“Watu wana wagonjwa wanashindwa kupanda magari kukiwa kuna mwendokasi watapanda kwenda hospitali,” ameongeza.
Chalamila mesema mabasi yaliyosajiliwa ni mengi, huku akieleza kuwa anaamini idadi ya madereva ni mara mbili ya mabasi yaliyopo hivyo kufanya uwezekano wa kufanya kazi saa 24 kwa kupishana.