RC Chalamila: Januari 24 wanajeshi watafanya usafi Dar es Salaam

0
37

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ametangaza kufanyika kwa zoezi kubwa la usafi katika Wilaya zote tano za mkoa huo kuanzia tarehe 23 hadi 24 Januari, mwaka huu, zoezi litakalohusisha wanajeshi, polisi, na vyombo vingine vya dola.

Ameyasema hayo katika ibada ya kuwekwa Wakfu Mwangalizi wa Jimbo la Babtist la Dar es Salaam, ambapo amewataka wakazi wa Dar es Salaam kutokuwa na shaka watakapoviona vyombo vya Dola vikifanya usafi kwani ni kwaajili ya kuliweka jiji salama.

Katika taarifa yake, RC Chalamila amewahakikishia wananchi wa Dar es Salaam kwamba zoezi hilo la usafi litakaloshirikisha wanajeshi zaidi ya 5000, polisi zaidi ya 3000, FFU na vyombo vingine vya dola, litakuwa ni jitihada za pamoja za kuboresha mazingira ya jiji na kupunguza hatari za magonjwa ikiwemo kipindupindu.

“Sisi Serikali tumeamua tarehe 23 na tarehe 24 tutafanya usafi katika mkoa mzima kwa kushirikiana na vyombo vya dola. Kwahiyo vyombo vya dola vitatapakaa katika Mkoa wetu wote, kwahiyo mkiona wanajeshi wengi barabarani tarehe 23 tarehe 24 msiogope mjue wanafanya usafi wa jiji la Dar es Salaam,” amesema.

Ameongeza kwamba magari mbalimbali ya kijeshi yatatumika kwa ajili ya kukusanya takataka katika siku hizo mbili.

Send this to a friend