RC Chalamila: Wanaopanga kuandamana waache mara moja

0
45

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila amewataka baadhi ya wananchi wanaopanga kuandamana wakidai kupinga ubia wa uendelezaji na uboreshaji ufanisi wa bandari kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya Dubai kuacha mara moja kwa kuwa si muda sahihi wa kufanya hivyo.

Akizungumza leo na waandishi wa Habari, amesema ameona taarifa katika mitandao ya kijamii  kuhusu baadhi ya watu kuwa na azma ya kuandamana mkoani Dar es Salaam leo kupinga makubaliano ya ushirikiano huo yakiongozwa na kijana Mwanaharakati wa Haki za Binadamu, Deusdedith Soka.

“Nimeona baadhi ya watu kuwa na azma ya kuandamana wakidai wanapinga kilichoamuliwa kuhusu ubia wa uendelezaji wa bandari kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai. [..] Tumeelekeza huu sio muda wa maandamano hata kidogo, jambo hili kwa mtu anayetaka kulifahamu kuna njia sahihi ya kulifahamu.

Ameongeza “Maandamano yanasitisha muda wa biashara na watu kupata huduma za haraka za hospitali, kwa mantiki hiyo vijana wote ambao wamekusudia kufanya haya basi waache mara moja.

Maandamano hayo yaliyoitwa ya amani yalipangwa kufanyika leo Juni 19, 2023 kuanzia Temeke kuelekea Magogoni Dar es Salaam ambapo taarifa za awali zinasema baadhi ya watu wamekamatwa baada ya kujitokeza kushiriki maandamano hayo.

Send this to a friend