RC Dar, Abubakar Kunenge akubali kuwa mlezi wa Harmonize na kundi lake

0
53

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge amekubali ombi la kuwa mlezi wa kundi la muziki la Konde Gang linaloongozwa na mwanamuziki Harmonize.

Akizungumza na wasanii na watendaji wengine wa kundi hilo, Kunenge amesema ana furaha kuwa mlezi wao, lakini amewataka wafanye mambo yatakayompa heshima.

“… mfanye mambo ambayo yataendana na heshima ya mkuu wa mkoa. Msifanye vinginevyo, ili nijivunie kuwa na ninyi nisije kulaumu nikasema kwamba, da! ningelijua.”

Amesema yeye kama mlezi kazi yake kubwa ni kulea vipaji na kuhakikisha wasanii hao wanapata mafanikio.

Ameongeza kuwa, sekta ya muziki imetoa ajira nyingi kwa watu mbalimbali, na hivyo amewapongeza wasanii wote nchi kwa namna wanavyojituma kuboresha maisha yao na kuchochea maendeleo.

“Kazi mnayofanya ya kulea vipaji ni kazi iliyotakiwa kufanywa na serikali lakini ninyi mnatusaidia,” amesema Kunenge kwa uongozi wa kundi hilo.

Amesema serikali itahakikisha inasimamia na kuboresha maslahi ya wasanii wote ili wanufaike na kazi zao za sanaa.