Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amesema amebaini kuwa mamlaka nchini Kenya zimekuwa zikitangaza kuwa madereva wa Tanzania wanaotaka kuingia nchini humo wana maambukizi ya virusi corona, jambo ambalo si sahihi.
Gambo amesema hayo na kueleza kuwa mbinu hiyo ya mamlaka za Kenya inalenga kuua soko la utalii mkoani Arusha na Tanzania kwa ujumla.
Katika taarifa yake aliyoitoa leo Mei 20, 2020 kiongozi huyo amesema amebaini hilo baada ya madereva 19 wa Tanzania waliotangazwa na Kenya kuwa na maambukizi kupimwa upya na kubainika hawana maambukizi ya virusi hivyo vibavyosababisha homa ya mapafu (Covid-19).
“Mkoa wa Arusha umejiridhisha kuwa hizi ni mbinu za nchi ya Kenya ili kuua soko la utalii mkoani Arusha na Tanzania kwa ujumla,” Gambo ameeleza kwenye taarifa yake ambayo Swahili Times imeiona.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa Mei 14, 2020 sampuli za madereva 44 mpakani hapo zilichukuliwa na kupelekwa Dar es Salaam katika maabara ya taifa ambapo majibu yanaonesha kuwa madereva 14 (11 wa Kenya, 1 wa Uganda na 2 kutoka nchi ambayo hakuitaja) kutoka Kenya walikutwa na maambukizi, huku 30 wakiwa hawana.
Amesema mkoa huo unaendelea kuchukua tahadhari kudhibiti maambukizi ya Covid-19 kupitia Mpaka wa Namanga unaoziunganisha Tanzania na Kenya.