RC Makonda atishia kumnyang'anya Meya wa Kinondoni fedha za maboresho ya Coco Beach

0
40

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda leo August 09 ametoa mwezi mmoja  kwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni na Mkurugenzi wa Manispaa hiyo kuhakikisha ujenzi wa maboresho ya fukwe za Coco unaanza mara moja na kama wakishindwa watanyang’anywa fedha hizo na kutafutwa mzabuni.

Mapema leo RC Makonda akiambatana na Katibu Tawala wa Mkoa huo wamefika kwenye ufukwe huo kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya mradi, lakini wameshangazwa kuona hakuna chochote kinachoendelea wakati tayari Rais Dkt. John Magufuli alishatoa kiasi cha Shilingi Bilioni 14 za ujenzi.

Amesema licha ya Rais kutoa kiasi fedha hizo, viongozi wameziweka tu kwenye akaunti bila matumizi huku watendaji wakilumbana kwenye vikao.

RC Makonda amesema kinachomsikitisha zaidi ni kuona mshauri wa mradi amebadili mchoro wa mwonekano mpya wa fukwe ambao ndio ulioombewa fedha kiasi cha TZS bilioni 14 na kuja mchoro wake mwingine wa TZS bilioni 40,bila kujua fedha hizo zitatoka wapi. Amesema kitendo hicho ni hujuma kwa serikali.

Aidha RC Makonda amewataka wananchi wajue kuwa kinachochelewesha mradi ni uzembe unaofanywa na watendaji wachache ambao wameishia kushinda kwenye vikao.

Pamoja na hayo RC Makonda amezitaka Halmashauri zote za mkoani humo kuhakikisha fedha zinazotolewa kwaajili ya maendeleo ya wananchi zinatumika na sio kuwekwa kwenye akaunti huku wananchi wakitaabika.

Send this to a friend