RC Singida aagiza kukamatwa kwa wanafunzi wa kike waliopata mimba

0
41

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego ameagiza kukamatwa kwa wanafunzi wa kike waliopata mimba wakiwa shuleni pamoja na wazazi wao na kuchukuliwa hatua za kisheria ili kukomesha tatizo hilo.

Amesema ili kukomesha tatizo hilo yeye ataanza kukamata kwanza msichana aliyepata ujauzito na baadaye atafuatia mvulana kama mtuhumiwa namba mbili ikiwa ni hatua ya kukomesha vitendo vya mimba kwa wanafunzi.

“Nikikuta msichana umepata mimba wewe utakuwa mshtakiwa namba moja na wewe ndio utakayekwenda jela bila huruma na tumbo lako utajifungulia huko huko kwa sababu mna tabia ya ukipata mimba tunaenda kukimbizana na mtoto wa kiume si sawa, wote mlishirikiana kwa hiyo yeye atakuwa mshtakiwa namba mbili na msichana atakuwa mshtakiwa namba moja,”amesema.

Aidha, amewapa muda wa mwezi mmoja makatibu tarafa na maafisa watendaji wa vijiji kuhakikisha wanawasaka na kuwarudisha wanafunzi 4,000 ambao hawajaripoti shuleni mpaka hivi sasa.

Ameongeza kuwa ni aibu kwa Serikali kujenga shule kwa gharama kubwa lakini wanafunzi hawaonekani shuleni, hivyo hatokubali aibu hiyo imkute pamoja na kusisitiza kupatiwa taarifa zote za wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ambao hawajaripo shuleni.

Send this to a friend