
Msanii nyota wa muziki nchini Nigeria, Divine Ikubor maarufu kama Rema, amesema kuwa wazazi wa Nigeria mara nyingi hufumbia macho maamuzi ya watoto wao iwapo watoto hao wanachangia kwa kiasi kikubwa katika familia.
Akiwa katika mazungumzo na mtayarishaji wa maudhui, Enzo, Rema amezungumza kuhusu jinsi mafanikio ya kifedha yanavyoweza kubadili mitazamo ya wazazi kuhusu maisha ya watoto wao.
Enzo alikuwa akielezea changamoto anayokumbana nayo kutoka kwa mama yake kuhusu uvaaji wa mitindo ya kisasa. “Mama yangu haniruhusu kuchora tattoo. Wakati niliposuka nywele, hakuzungumza nami kwa siku kadhaa, ilikuwa mbaya,” amesema.
Akijibu, Rema alimshauri Enzo kuendelea kujitahidi ili kupata mafanikio zaidi, akisema: “Usijali, unahitaji tu kujituma zaidi. Subiri pale utakapopata hela nyingi. Wazazi wa Nigeria hawawashauri wanaowalisha.”
Rema pia amefichua kuwa tangu akiwa kijana amekuwa mtegemezi mkuu wa familia, hasa baada ya kufariki kwa baba yake. Amesema alipata milioni yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 17 na akaikabidhi yote kwa mama yake.
Kauli ya Rema imezua mjadala mtandaoni na wengine wakikubaliana naye kuhusu hali halisi ya familia nyingi barani Afrika ambapo mafanikio ya kifedha huleta heshima ya haraka nyumbani.