Ripoti: Simu za Tecno zinavyoiba fedha za watumiaji wake

0
39

Licha ya janga la corona kuendelea kuwa na athari kiuchumi duniani, kampuni ya Transsion Holdings kutoka China imeripoti ongezeko la faida kwa 33% katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020. Usafirishaji wa simu zake (TECNO) umeongezeka kwa 32% mwaka kwa mwaka katika robo ya pili ya mwaka 2020, ambapo kampuni hiyo inashikilia soko la chini na la kati barani Afrika.

Lakini faida hiyo inadaiwa kuwa imepatikana kwa njia inayotia wasiwasi ambapo ripoti inaonesha kuwa maelfu ya simu zake zimeuzwa zikiwa na programu yenye uwezo wa kupakua (download) na kumuunga mtumiaji katika huduma za kulipia bila yeye mwenyewe kujua.

Utafiti uliofanywa na Secure-D, kampuni ya huduma za ulinzi wa simu inayomilikiwa na Upstream, umebainisha kuwa kati ya Machi hadi Disemba 2019 teknolojia yake ilizuia miamala 844,000 iliyohusishwa na programu inayowekwa kwenye simu hizo kabla ya kuuuzwa.

Pia, Secure-D imesema kuwa imezuia uungwaji katika huduma za kulipia mara milioni 19.2 kati ya Machi 2019 hadi Agosti 2020, ambapo shughuli hizo zilikuwa zikifanyika katika simu 200,000 aina ya Tecno W2 kutoka nchi 19, nyingi zikiwa za Afrika ikiwa ni pamoja na Misri, Ethiopia, Afrika Kusini, Cameroon na Ghana, na kuwa shughuli hiyo haramu unaendelea.

Licha ya kuwa watumiaji wengi wa Tecno wanaweza wasifahamu uwepo wa programu hiyo, lakini muda wao wa maongezi na vifurushi vya intaneti huisha haraka kuliko kawaida kwani vinatumika kuungwa kwenye huduma za ulipiaji kupitia programu hiyo ambayo hutuma fedha kwa Transsion, kampuni inayotengeneza simu hizo.

Hata hivyo, Transsion imesema kuwa simu aina moja tu kati ya aina mbalimbali za simu zake ndiyo imeathirika na tayari maboresho ya kurekebisha tatizo hilo yameshatolewa. Hata hivyo, kampuni hiyo haijaeleza ni watu wangapi wamepakua ‘patch’ ya kurekebisha kasoro hiyo au kama iliwataarifu watumiaji wake kama walikuwa wameathiriwa.

Tangu kuanzishwa kwake, Transsion imefanikiwa kuliteka soko la Afrika kwa kuuza simu kwa bei nafuu ikilinganishwa na makampuni makubwa Samsung na Apple ambayo tayari yalikuwa sokoni. Nusu ya simu zinazotengenezwa na kampuni hiyo huuzwa barani Afrika.

Licha ya Transsion kueleza tatizo hilo limetatuliwa, lakini ni wazi kuwa kampuni hiyo itaathirika hasa kwa baadhi ya watumiaji kutokuwa na imani na bidhaa zake.

Send this to a friend