Ripoti ya Mei 2024 ya Benki Kuu ya Tanzania iliyotolewa Juni 17, imeonesha kuwa sekta ya utalii imeendelea kukua kwa kiasi kikubwa kwa idadi kubwa ya watalii wanaofurika kuja nchini.
Ripoti imeonesha kwa Machi na Aprili mwaka huu watalii wa kimataifa wameongezeka kwa asilimia 21.9 na 21.8 mtawalia ikilinganishwa na miezi kama hiyo mwaka jana, hali inayoonesha kuendelea kuimarika kwa sekta ya utalii nchini na duniani.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa katika miezi hiyo pia, sekta ya utalii imeingiza fedha za kigeni Dola za Marekani bilioni 3.58 na bilioni 5.75 kwa mwezi Machi na Aprili mwaka huu kutoka Dola Bilioni 2.7 na bilioni 2.8 kwa miezi kama hiyo mwaka jana huku Sekta inayofuatia ikiwa ni madini iliyofikia Dola bilioni 3.1 Aprili mwaka huu na Uchukuzi ikiwa na Dola bilioni 2.5.
Mafanikio hayo makubwa yanatajwa kuchangiwa na Filamu ya ‘The Royal Tour’ aliyoshiriki Rais Samia Suluhu pamoja na mwamko wa Serikali na wadau wa sekta binafsi katika kujitangaza kimataifa.
Ripoti ya BoT inaonesha kuunga mkono utafiti mwingine uliofanywa na Shirika la Utalii Duniani kwa robo ya mwezi Januari hadi Machi, 2024, ambapo kwa ukuaji unaoendelea sasa wa sekta ya utalii nchini, Tanzania ilishika nafasi ya kwanza Afrika na ya nne duniani kwa ongezeko kubwa la watalii ikilinganishwa na kabla ya UVIKO-19 yaani mwaka 2019.