
Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imeonesha kuwa kulikuwa na upendeleo mkubwa wa kikabila upande wa ajira katika ofisi ya aliyekuwa Naibu Rais wa Kenya, Rigathi Gachagua wakati wa uongozi wake.
Mkaguzi Mkuu, Nancy Gathungu amesema kwa mwaka wa Fedha 2023/2024, alibaini kuwa kati ya wafanyakazi 542 katika ofisi hiyo, wafanyakazi 249 sawa na asilimia 46 walitoka katika jamii moja.
“Hii ni kinyume na Kifungu cha 7(1) na 7(2) cha Sheria ya Uwiano wa Kitaifa na Ujumuishaji ya mwaka 2008, ambayo inasema kuwa taasisi zote za umma zinapaswa kuwakilisha utofauti wa wananchi wa Kenya katika ajira zao, na hakuna taasisi yoyote ya umma inayopaswa kuwa na zaidi ya theluthi moja ya wafanyakazi kutoka jamii moja,” inasema ripoti hiyo.
Ameongeza kuwa katika kipindi hicho, pia kilibaini kuwa watumishi 42 walipokea mishahara yote chini ya theluthi moja ya mishahara yao katika miezi tofauti, na kukiuka masharti ya Kifungu cha 19 (3) cha Sheria ya Ajira, 2007 kinachoamuru kwamba makato yote yanayotokana na mishahara ya wafanyakazi yasizidi theluthi mbili ya mishahara yao.
Ofisi hiyo pia ilikuwa na madeni ya Ksh. milioni 4.8 [TZS milioni 96.5] ambayo hayakulipwa hadi kufikia Juni 30, 2024, na badala yake madeni hayo yalipelekwa kwenye bajeti ya mwaka wa Fedha wa 2024/2025.
Gathungu ameeleza kuwa kushindwa kulipa madeni hayo kulisababisha mgongano katika upangaji wa bajeti kwa mwaka uliofuata. Pia alisisitiza umuhimu wa uwajibikaji na usiri katika matumizi ya fedha za umma huku akipendekeza marekebisho ya kanuni ili kuweka wazi matumizi yanayoongozwa na masuala ya usalama.