Ripoti ya Mto Mara yadaiwa kupotosha ukweli

0
54

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kikishirikiana na Chama cha Mazingira kwa Vitendo (Leat) wametoa Wito kwa Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango kuunda tume huru ya uchunguzi itakayowajumuisha wanamazingira mahiri na wenye weledi mkubwa kutoka ndani na nje ya nchi ili kuchunguza tena uchafuzi wa Mto Mara.

Taarifa iliyotolewa na kamati maalumu ya uchunguzi iliyoundwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dkt. Suleimani Jafo imedaiwa kuwa imepotosha ukweli.

Akizungumza na gazeti la Mwanachi Waziri Jafo amesema kuwa Serikali ndiyo kwanza imepokea taarifa kutoka kwa kamati hiyo, hivyo itafanyiwa uchambuzi wa kina na kisha kutolewa maelekezo, kwa sasa hawezi kutoa majibu ya moja kwa moja lakini wanaendelea kupokea maoni ya wadau kuhusu hilo.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga katika mkutano wake na waandishi wa habari jana jijini Dar es salaam amesema kuwa, taarifa iliyotolewa na Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria ilisema kuwa uchafuzi huo ulitokana na grisi, na taarifa ya kamati ya Profesa Samwel Manyele ilihusisha uchafuzi huo na vinyesi na shughuli zingine za kibinadamu.

Aidha, anaelezea namna walivyofanya utafiti kuhusu suala hilo na kutembelea maeneo ya wakazi wanaoishi jirani na mto huo na kubaini mambo mbalimbali ikiwemo kuwepo kwa vifo vya mifugo ya wakazi wa maeneo hayo.

“Ilibainika katika kipindi cha mwaka 2018 hadi 2022 zaidi ya mifugo 800 ilikufa kwa kunywa maji yanayodhaniwa kuwa na sumu yanayopatikana katika bonde la Mto Mara, na katika kipindi cha kati ya tarehe 1 hadi 15 Machi mwaka huu, zaidi ya ng’ombe 54 waliripotiwa kufa,” amesema Henga.

Alidai taarifa hizo zimebaini kuwa kati ya mwaka 2020 mpaka 2021 kumekuwa na matukio ya wakazi wa maeneo hayo jirani na mto huo kukumbwa na ugonjwa wa ngozi unaowafanya kuwashwa ngozi na kujikuna kupita kiasi na hata kutumia vifaa kama miti na magunzi ya mahindi ili kupunguzi miwasho, ambapo ugonjwa huo ulipewa jina linalofahamika kama ‘kwangua vocha.’

Send this to a friend