RPC Kagera aliyesema anataka kuwa IGP arejeshwa Makao Makuu ya Polisi, Dodoma

1
85

Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro amemrejesha Makao Makuu ya Polisi, Dodoma Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Wankyo Nyigesa.

Kufuatia mabadiliko hayo, nafasi yake inachukuliwa na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), William Mwampagale

Uhamisho huo umefanyika ili kupisha uchunguzi wa tukio la Machi 26, 2022 katika sherehe ya kumuaga Nyigesa ambaye alihamishwa kutoka Pwani kwenda Kagera, na nafasi yake kuchukuliwa na Pius Tuli.

Kwa mujibu wa Polisi, maneno aliyoyatoa yameonesha ukiukwaji wa nidhamu kulingana na miongozi ya Jeshi la Polisi, na kwamba suala hilo limeanza kufanyiwa kazi na hatua zaidi zitachukuliwa.

Licha ya kuwa taarifa ya polisi haijaeleza maneno yaliyotolewa, lakini hivi karibuni kamanda huyo alisikika akisema kwamba sasa anajiandaa kuwa IGP.

“Mimi huwa ninajiandaa kuwa DCI [Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai] lakini nafasi ya DCI ikachukuliwa, nikajiandaa kuwa Kamishna wa [Polisi] Zanzibar, Kamishna wa [Polisi] Zanzibar wakachukua, sasa hivi najiandaa kuwa IGP,” alisema Wankyo.

Aliongeza kwamba anatamani Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Samia Suluhu Hassan amteue ashike nafasi hiyo kwani anaamini atafanya makubwa, na anataka kufanya kazi kwa miaka mitatu tu.

Kufuatia mabadiliko hayo, aliyekuwa Afisa Mnadhimu Mkoa wa Rukwa, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Theopista Mally anakuwa Kamanda wa Polisi wa mkoa huo.